Serikali ya Kaunti ya Nakuru imejiunga na kaunti zingine zinazokuza majani chai kushinikiza kutekelezwa kwa haki za wakulima wa majani chai.
Gavana wa Nakuru Kinuthia Mbugua alijiunga na Magavana wengine kutoka Kericho Profesa Paul Chepkwony, Peter Munya wa Kaunti ya Meru, Mwangi Wa Iria wa Murang'a na Joseph Ndathi wa Kirinyaga kwa lengo hilo.
Magavana hao wamesema kuwa Serikali ya kitaifa imeifanya sekta hiyo kufifia kwa sababu ya ukosefu wa mbinu bora za ustawi wa sekta na kutozwa ushuru zaidi.
Magavana hao pia walisema kuwa sekta ya kilimo imegatuliwa kabisa na kupitia kwa wakulima wameweza kujua masaibu yanayokumba wakulima.
Gavana wa Kaunti ya Kericho Profesa Paul Chepkwony alisema kuwa tayari ametayarisha mswada utakao husisha Magavana wote kutathmini jinsi ya kuiboresha sekta hiyo ya mabilioni ya pesa na kumnusuru mkulima wa kawaida.
Kaunti ya Kericho ndio inayoongoza nchini kwa kutoa majani bora ya kuuza ng'ambo.
Kilimo cha majani chai nchini Kenya ni miongoni mwa biashara zinazofanywa na mataifa ya kigeni na huletea nchi ya Kenya faida kubwa.