Kaunti ya Nakuru inatarajiwa kutumia Sh500m katika harakati za kujitayarisha kukabiliana na mvua kubwa ya El Nino.
Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua alisema kuwa kutokana na gharama ya zoezi hilo, huenda ikapelekea baadhi ya fedha zilizotengewa miradi mingine kuelekezwa katika shughuli za kuzuia madhara ambayo huenda yakatokana na mvua hiyo inayotarajiwa kunyesha mwezi huu.
Akizungumza siku ya Alhamisi alipokuwa akizindua rasmi kamati ya Kaunti ya Nakuru ya kupanga mikakati ya kujikinga na madhara ya mvua hiyo katika kituo cha kutoa mafunzo ya kilimo kilicho Soilo, Mbugua alisema kuwa lengo la kufanya mkutano huo ni kuhakikisha mipango ya kujikinga na madhara ya mvua hiyo ya El Nino ni mwafaka.
“Huu si mkutano wa kwanza kwani tumekuwa tukifanya mikutano kwenye sekta mbalimbali na pia tumehudhuria mikutano mingine jijini Nairobi, chini ya kitengo cha kitaifa cha kukabiliana na majanga,” alisema Mbugua.
Gavana Mbugua pia alionyesha kuridhishwa kwake na yale yaliyotokana namkutano huo ambao ulijumuisha washikadau wote.
Kuhusiana na jinsi kaunti imejitayarisha kwa mvua hiyo, Gavana Mbugua alisema hatua hiyo inafaa kuwa miongoni mwa mipango inayojumuishwa katika kuendeleza shughuli za kaunti.
“Majanga huenda yakazuka wakati wowote ule. Kwa hivyo, ni lazima tuangalie njia za kufanya yale ambayo tumeanza leo yadumu kwa sasa na katika siku za usoni,” alisema Mbugua.
Kando na kubuni jopo hilo, mkutano huo pia ulilenga kubaini maeneo ambayo huenda yakaathiriwa pakubwa na mvua hiyo ya El Nino katika Kaunti ya Nakuru kama vile maeneo yaliyo karibu na Ziwa Naivasha, Elementaita na Nakuru.