Katibu wa kudumu kwenye Wizara ya Kilimo Profesa Fred Segor amesema ili uchumi wamataifa yanayo endelea kustawi barani Africa kuimarika, sharti mataifa hayo yazingatie kilimo endelevu ili kujistawisha zaidi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza kwenye hafla yakuadhimisha siku ya chakula duniani kule Rigoma, Kaunti ya Nyamira, Segor alisema kuwa serikali ya kitaifa imeipa sekta ya kilimo kipau mbele kwa kuwapunguzia wakulima kote nchini bei ya mbolea.

"Serikali ya kitaifa imeipa sekta ya kilimo kipau mbele kwa kuwapungumzia wakulima kote nchini bei ya mbolea mwaka huu ili kuwawezesha kuendeleza shughuli zao za kila siku,” alisema Segor.

Katibu Segor aidha alisema kuwa swala la uwepo wa chakula cha kutosha nchini ni la muhimu kwa kuwa watu millioni 1.5 hutegemea chakula cha mswada swala linalofaa kuangaziwa kwa dharura.

Kwa upande wake Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama alisema kuwa asilimia 90 ya wakazi wa Kaunti ya Nyamira hutegemea sana kilimo kama njia mojawapo yakujiendeleza kimaisha.

"Asilimia 90 ya wakazi wa Nyamira hutegemea kilimo kama njia mojawapo yakujiendeleza kimaisha na kwa sababu hiyo, serikali yangu ilitenga kiwango kikubwa cha fedha kwenye makadirio ya bajeti mwaka huu ili kuwawezesha wakulima kuendeleza na shughuli zao,” alisema Nyagarama.

Naibu Gavana wa kaunti hiyo Amos Nyaribo alimwomba Segor kuwasilisha ujumbe kwa Rais Kenyatta kutupilia mbali kodi inayotozwa bidhaa za kilimo nchini.