Serikali ya Kaunti ya Nyamira imeweka mikakati kabambe ya kuinua kilimo katika kaunti hiyo haswa kutafutia wakulima soko kwa mazao yao.
Akizungumza siku ya Alhamisi mjini Nyamira, afisa wa kilimo katika kaunti hiyo Edward Ondigi alisema serikali ya kaunti ya Nyamira itaunganisha wakulima wote ili kuinua kilimo katika kaunti hiyo.
“Serikali ya kaunti yetu ya Nyamira imeweka mikakati ya kuhakikisha kilimo kimeinuka, na tutatafutia wakulima wetu soko ili kuuza mazao yao,” alisema Ondigi.
Wakulima wa kaunti hiyo walikuwa wameomba serikali hiyo kuwakumbuka haswa kwa kuwatafutia soko, jambo ambalo sasa limejibiwa.
Kwa upande wa wakulima hao, walifurahia jambo hilo na kusema sasa huenda kilimo kipewe kipau mbele zaidi.
“Sisi wakulima wa majani chai tumekuwa tukipata pesa kidogo kwa kila kilo ya majani chai, sasa tunaomba serikali ya kaunti yetu kuendelea kutusaidia jinsi tumesikia na tutafutiwe soko ili tuwe tunafaika na mumea wa majani chai,” alisema Alfred Monari, mkulima wa majani chai.