Zaidi ya taa mia tatu zinazotumia miale ya jua zimewekwa katika maeneo mbalimbali ya Kaunti ya Nakuru kama vile mjini Naivasha na eneo la Nakuru Magharibi.
Akizungumza kwenye hafla ya kuzindua rasmi mradi wa kuweka taa za mitaani zinzotumia miale ya jua siku ya Jumatano katika eneo la Manyani viungani mwa mji wa Nakuru, Mkuu wa Idara ya Barabara na Usafiri kwenye Kaunti ya Nakuru Joel Maina alisema mradi huo ungali unaendelea.
Maina alisema mradi huo utasaidia kaunti hiyo kupunguza gharama ya matumizi inayotokana na nyaya za nguvu za umeme.
Aidha, alisema kwamba mradi huo pia utasaidia katika kutumia rasilmali inayopatikana kwa njia ya kiasili (natural resources) kwa njia ifaayo.
Uzinduzi huo wa taa hizo zinazotumia miale hiyo ulifanyawa na Gavana wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua.
Gavana alikuwa ameandamana na Naibu wake Joseph Ruto, Afisa mkuu katika kitengo cha kilimo, mifugo na uvuvi Wanja Muritu, mwakilishi wa wadi ya biashara Steve Kuria miongoni mwa maafisa wengine kwenye serikali ya kaunti ya Nakuru.