Serikali ya kaunti ya Kisii imeaswa kuwaondoa watoto wa kurandaranda mitaani al maarufu ‘Chokoraa mjini.
Hii ni baada ya watoto hao kudaiwa kuhusika katika wizi mjini humo jambo ambalo limekemewa vikali na serikali ya kaunti sasa imeombwa kuwaondoa.
Akizungumza hii leo mjini Kisii katibu wa wafanyibiashara katika Soko la ‘Market’ lililoko katikati mwa mji, Nemuel Mwalimu alisema serikali ya kaunti huwa inatenga pesa kila mwaka za kuwashughulikia watoto hao huku akiomba serikali hiyo kuwaondoa na kuwapeleka shule watoto hao.
Mwalimu alisema serikali ilitenga pesa za kuwajengea watoto hao katika eneo la Kiamuasi, akisema hilo lifanyike haraka kwani watoto hao wameanza kuwa kero kwa wakaazi wa mjini.
“Hatuna vile tutawaondoa watoto hawa sisi wenyewe tunaomba serikali ya kaunti ya Kisii kupitia gavana wetu kushughulikia mambo hayo,” alisema Mwalimu.