Serikali ya Kaunti ya Mombasa imekaidi amri ya kuwaondoa maafisa wa kaunti barabarani.
Haya yanajiri baada ya kamanda mkuu wa Nyali kuimarisha idara ya trafiki katika kaunti hito kuwaondoa maafisa hao wa kaunti barabarani maramoja.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa, mkuu wa idara hiyo Tawfiq Balala alisema kuwa kamwe hawawezi kufuata amri hiyo, kwa kuwa haikuwasilishwa kwa njia ifaayao.
Balala alisema kuwa hatua ya kuwaamuru maafisa hao kusitisha majukumu yao bila ya kutoa sababu ya kimsingi, ni ukiukaji wa Katiba ya nchi.
Balala alisema kuwa maafisa hao wamesaidia pakubwa katika kukabiliana na msongamano wa magari katika jiji la Mombasa.
Aidha, alisema kuwa maafisa hao wa kaunti wamepokea barua rasmi kutoka kwa mamlaka ya uchukuzi na usalama barabarani nchini NTSA, ya kuwapongeza kwa utendakazi wao bora hasa wakati wa msimu Krismasi.
“Endapo maafisa hao watasitishwa kutekeleza majukumu yao, hatua hiyo itachangia kushuhudiwa kwa msongamano mkubwa Mombasa,” alisema Balala.
Wakati huo huo Balala amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kuwa vita vya kisiasa kati ya serikali kuu na Gavana Hassan Joho vinaingilia utendakazi wa idara hiyo.
Alisema kuwa wamefanya maongezi ya kina na Gavana Joho na akawaamrisha kutofuata amri hiyo na kuendelea na shughuli zao kama kawaida.