Mwenyekiti wa kikundi cha ngoma za kitamaduni cha Kimuri, Joyce Ndungu, ameitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kutafuta wafadhili wataowezesha wasanii mbali mbali kunufaika na mauzo ya usanii wa kitamaduni.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Mombasa, Bi Ndungu alisema kuwa mipangilio bora itawawezesha wafadhili kujitokeza na kuongeza mauzo, hivyo kuwapa wasanii biashara mbadala za kukimu maisha.
Ndungu alisema kuwa serikali ya Kaunti ya Mombasa inapaswa kuzingatia usanii wa kitamaduni miongoni mwa vijana, ili kupunguza visa vya utovu wa nidhamu.
Haya yanajiri baada ya Tamasha la Tukutane Mombasa kufanyika mapema wiki iliyopita na kufika kilele siku ya Jumamosi, huku kiongozi wa muungano wa Cord Raila Odinga akishiriki katika tamasha hilo.
Odinga alisema kuwa tamasha hilo liliunganisha Wakenya kutoka makabila mbali mbali na kuendeleza mipangilio ya ugatuzi nchini.
Wakaazi mbali mbali wanatarajia viongozi nchini kutathmini mipangilio itakayowawezesha kuboresha maisha yao ili kufaidi mipangilio ya ugatuzi.