Serikali ya Kaunti ya Mombasa imekosolewa na watalaam wa kiafya kwa kushindwa kuboresha mazingira ya wakaazi na kuchangia kuzuka kwa maradhi ya kiafya kama vile homanyongo.
Mtaalam wa maradhi ya kiakili mjini Mombasa Edwin Chokwe amesema kuwa mji wa Mombasa umekosa mpangilio wa ujenzi na hata kukosa mitaro ya kupitisha maji taka.
Alisema kuwa hali hiyo husababisha maji taka kuchanganyikana na maji ya visima ambayo wakaazi hutumia kwa matumizi ya nyumbani.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Chokwe alisema kuwa lazima hatua mwafaka zichukuliwe na idara ya mazingira katika kaunti hiyo, ili kuokoa wakaazi ambao huenda wakaathirika kiafya kufuatia mazingira duni na uchafu uliotanda mjini Mombasa.
"Ni lazima swala la maji taka kusuluhishwa mara moja kwani hali hiyo huenda ikasababisha maradhi hasa ikizingatiwa kuwa maradhi mengi huchipuka msimu wa mvua,” alisema Chokwe.
Mtaalam huyo wa maswla ya afya alisema kuwa wakaazi wako katika hatari zaidi ya kuambukizwa maradhi ya kiafya ikiwemo kuchipuka kwa ugonjwa wa kipindupindu, kufuatia kufurika kwa mitaro ya maji.
Chokwe ameitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kuhakikisha kuwa mabomba ya maji taka yamerekebishwa ili maswala ya kiafya kuangaziwa vyema.