Serikali ya kaunti ya Kisii imehimizwa kutenga pesa na kujenga makaazi ya watoto wa kurandaranda mitaani almaarufu chokoraa.
Akizungumza siku ya jumanne katika uwanja wa Gusii stadium wakati wa kusherekea siku ya chokoraa mtetezi wa watoto hao wa kurandaranda Joel Machuka aliomba serikali ya kaunti ya Kisii kujenga makao ya watoto hao ili kuwaondoa mitaani.
Kulingana naye tayari kuna eneo la kujengwa maakazi katika eneo la Kiamwasi na kuomba serikali kutenga pesa ili kuwajengea watoto hao makaazi.
“Katika miji tofauti tofauti iliyoko katika kaunti ya Kisii unapata kuna watoto wa kurandaranda na wanastahili kusaidiwa ili kuondoka mitaani,” alisema Machuka.
“Mji wa Kisii pekee unaandikisha zaidi ya watoto wa kurandaranda 200 na ninaomba serikali ya kaunti kujaribu kila iwezalo na kutenga kiwango fulani cha pesa ili kujenga maakaazi ya watoto hao katika eneo la Kiamwasi,” aliongeza Machuka.