Serikali ya kaunti ya Kisii imehimizwa kushirikiana na serikali ya kitaifa kuhakikisha wanachama wa polisi jamii wamepewa bidhaa husika wanapoimarisha usalama katika vijiji mbalimbali katika kaunti hiyo.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa wanachama hao hutumia bidhaa zao kuimarisha usalama kando na kusaidiwa na serikali .
Wakizungumza siku ya Jumatano katika eneo la Nyosia eneo bunge la Nyaribari chache kaunti ya Kisii wanachama hao wakiongozwa na Fredrick Ratemo waliomba serikali ya kaunti ya Kisii kujaribu kila iwezalo kuhakikisha wamepata usaidizi ili kuimarisha usalama nyakati za usiku.
Miongozni mwa bidhaa ambazo wanachama hao walipendekeza kukabidhiwa na serikali ni kurunzi (tochi) na viatu aina ya gumbuti.
“Tumekuwa tukijitolea kuimarisha usalama kila wakati katika vijiji mbalimbali bila kusaidiwa na serikali tunaomba serikali yetu ya kaunti ya Kisii kutusaidia ili tuwe na bidhaa muhimu tunapoimarisha usalama,” alisema Ratemo.
Aidha, wanachama hao waliomba serikali ya kitaifa kuwapa senti kidogo kama mshahara ili nao waweze kujikimu na kujiendeleza kimaisha.