Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi ameelezea haja ya eneo bunge lake kuwa na gari la zimamoto ili kukabiliana na majanga pindi yanapotokea.
Mwinyi amesema kuwa licha ya majengo ya nyumba katika eneo hilo kujengwa bila mpangilio, kuna haja ya eneo hilo kuwa na gari la kuzima moto.
Mbunge huyo amesema kuwa zaidi ya nyumba 30 zimeathirika na mikasa ya moto tangu mwaka wa 2013, na kuahidi kuhimiza wahusika kuweka kituo cha zimamoto katika eneo hilo, ili kukabiliana na hali hiyo.
"Tunaitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kuwa na mipango maalum na kuweka gari la zima moto Changamwe ili kukabiliana na majanga ya moto pindi yanapotokea,” alisema Mwinyi, siku ya Jumatatu.
Wakati huo huo, ameitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kukarabati barabara pamoja na kurekebisha ujenzi wa nyumba katika eneo hilo, ili kuwe na nafasi ya magari ya zima moto kupita na kudhibiti majanga pindi yanapotokea.
Kauli ya Mbunge huyo wa Changamwe inajiri huku visa vya moto vikiendelea kushuhudiwa humu nchini hasa katika shule za umma.