Mbunge wa Likoni Masuod Mwahima ameitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kuweka magari ya zimamoto katika kituo kipya kilichoko katika eneo la Shika Adabu, ili kuwasaidia wakaazi kukabiliana na mikasa ya moto.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Mwahima alisema kuwa wakaazi wa eneo hilo hupata shida ya kukabiliana na majanga ya moto punde yanapotokea kufuatia ukosefu wa vifaa katika kituo hicho.
Mbunge huyo alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kwa serikali ya kaunti kupeleka gari la taka katika kituo hicho badala ya gari la zimamoto.
Hata hivyo, Mwahima ameshinikiza serikali ya kaunti kuweka bayana iwapo imeshindwa kuliwajibikia swala hilo.
Alielekezea kidole cha lawama kwa wawakilishi wa wadi wa eneo bunge hilo kwa kucheleweshwa kuletwa vifaa hivyo katika kituo hicho.
Alidai kuwa wawakilishi hao hawashughuliki katika kupigia debe jambo hilo wakati wa vikao vyao katika bunge la kaunti.
"Tunaitaka serikali ya kaunti ya Mombasa kuhakikisha kuwa inaleta magari ya zimamoto ndio wakaazi wa eneo la Likoni waweze kukabiliana na majanga hasa wakati wa mikasa ya moto. Kama wameshindwa kutekeleza hayo, basi watwambie ili tutafute usaidizi kutoka kwa serikali kuu,” alisema Mwahima.