Serikali ya Kaunti ya Mombasa imetakiwa kujizatiti katika kuwatambua kikamilifu watu wanaoishi na ulemavu katika kaunti hiyo, na kubadili hali yao ya maisha.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwakilishi wa watu wanaoishi na ulemavu katika Bunge la Kaunti ya Mombasa Hurdson Karume, amesema kuwa jamii ya walemavu katika kaunti hiyo imekumbwa na changamoto nyingi mno za maisha, ambazo zinapaswa kutatuliwa ili kutoa mazingira bora kwa jamii hiyo.

Akizungumza katika mkutano wa viongozi wa watu wanoishi na ulemavu mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Karume alisema kwamba ni muhimu kwa jamii hiyo ya walemavu kuhusishwa na kutengewa miradi mbalimbali itakayowawezesha kujikimu kimaisha.

Aidha, alisisitiza kubadilishwa kwa hali duni ya maisha na vikwazo vingi vya kiuchumi wanavyopitia walemavu, ili kuwawezesha kujihusisha na shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kujikimu kimaisha.

"Tunaiomba serikali ya Kaunti ya Mombasa kuwatambua walemavu na kuwahakikishia mazingira bora," alisema Karume.

Hatua ya Karume inajiri siku chache tu baada ya jamii ya walemavu katika eneo la Bamburi na Changamwe kulalamikia kubaguliwa na serikali na kaunti.