Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Katibu wa Kaunti ya Mombasa Francis Thoya amekana madai kuwa serikali ya kaunti hiyo imetumia vibaya pesa zilizotengwa na serikali kuu kukabiliana na majanga wakati wa na mvua ya El Nino.

Kwenye mahojiano na idhaa ya redio moja mjini Mombasa siku ya Jumanne, Thoya alisema kuwa pesa hizo zinazokisiwa kuwa shilingi milioni 70 zimeelekezwa kwa matumizi katika idara zingine kwa kuwa kaunti hiyo haikushuhudia janga kubwa wakati wa mvua hiyo.

Thoya aidha alieleza kuwa walilazimika kuchukua hatua hiyo kwa kuwa pesa hizo zilikuwa zimekaa bila kutumika.

Hata hivyo, alisema kuwa watarejesha fedha hizo pindi watakapopokea mgao wa fedha wa kila mwaka kutoka kwa serikali ya kitaifa.

Kiongozi huyo vilevile alisema kuwa serikali ya kaunti imeweka mikakati dhabiti kuwalinda wananchi wake iwapo kutatokeoa janga lolote kufuatia mvua inayonyesha katika baadhi ya sehemu mjini Mombasa.

“Tumetenga kumbi katika kila kaunti ndogo hapa Mombasa ambazo zitatumika na wakaazi iwapo nyumba zao zitalowa maji kutokana na mvua inayoshuhudiwa hapa Pwani,” alisema Thoya.

Kauli ya Thoya inajiri siku chache tu baada ya baadhi ya viongozi kudai kuwa serikali ya kaunti imefuja pesa zilizotengwa kukabili janga la El Nino.