Shirika linalohusika na maswala ya watu wanaoishi na ulemavu mjini Mombasa 'Coast Association of Persons Living With Disabilities’, limekosoa namna oparesheni ya kufurusha familia zinazoishi mitaani inavyoendshwa.
Afisa mratibu wa shirika hilo Hamisa Zaja amesema maafisa wa kaunti wanaoendesha oparesheni hiyo wanawahangaisha walemavu wanaofanya biashara katika barabara za mji.
“Kama shirika hatutanyamaza huku watu wanaoishi na ulemavu wakihangaisha pasi na kufanya lolote. Ikiwa serikali haiwataki watu hawa kuishi na kufanya biashara yao mjini, basi watumie mbinu isiyokiuka haki zao,” alisema Bi Zaja.
Zaja alisema tangu oparesheni hiyo ianze, wamepokea malalamishi kutoka kwa watu kadhaa wanaoishi na ulemavu, huku wengine wakifikishwa na hata kuzuiliwa rumande na mali yao kuchukuliwa.
Zaja amependekeza serikali ya kaunti kubuni mfumo dhabiti wa kuondoa jamii zinazorandaranda barabarani, ambao hautaathiri wala kuwatatiza walemavu mjini humo.
Haya yanajiri huku mashirika ya kutetea haki za binadamu mjini Mombasa yakiongozwa na shirika la Huria yakipinga hatua ya serikali ya Kaunti ya Mombasa ya kuwafurusha vijana wanaorandaranda mtaani, kwa madai kuwa wanachangia kudorora kwa usalama.