Naibu gavana wa kaunti ya Kisii Joash Maangi amesema serikali hiyo itajenga maktaba za vitabu vya kusoma katika kila eneo bunge, ili kuinua viwango vya elimu.
Akizungumza siku ya Alhamisi wakati alipokuwa akifungua duka la kuuza vitabu vya kusoma la kaunti maarufu, County Distribution Centre Bookshop Limited, Maangi alisema serikali ya kaunti hiyo itajaribu kila iwezalo kuhakikisha viwango vya elimu vimeinuka kutoka mahala vilipo kwa sasa, kwa kujenga maktaba ya vitabu katika maeneo bunge yote tisa yaliopo kwa kaunti hiyo.
Aidha, Maangi aliomba kampuni za kutengeneza vitabu vya kusoma kufadhili kaunti hiyo vitabu vya kusoma ili kusaidia maktaba ambazo zitajengwa kuwa na vitabu vya kutosha.
“Serikali yetu ya kaunti itajenga maktaba za vitabu katika maeneo bunge yote tisa hapa Kisii ili kuinua viwango vya elimu na iweze kung’ara kote nchini katika sekta ya elimu,” alisema Maangi.
“Natoa wito kwa kampuni za kutengeneza vitabu vya kusoma nchini ziweze kutusaidia kwa kutufadhili vitabu vya kusoma ambavyo tutaviwekaza katika maktaba tutakazojenga ili ziwe na vitabu vya kutosha," aliongeza Maangi.
Aidha, Maangi aliomba wazazi kuwasomesha watoto wao ili waje kujisaidia nyakati za usoni kwani elimu ndio msingi wa kuleta maendeleo.