Serikali ya kaunti ya Nyamira imeombwa kutenga pesa kwa akina mama kuwasaidia kujiendeleza kupitia biashara.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa pesa zile ambazo hutolewa katika vikundi mbalimbali hazitoshi, huku akina mama wakiomba kutengewa pesa zao kando na zile za vikundi vya kila aina.

Wakizungumza siku ya Jumanne mjini Nyamira, akina mama hao wakiongozwa na Cicilia Moraa walisema pesa zile wanapata kupitia vikundi ni kidogo, na hazitoshi vikundi vingi. 

Wakati huo huo, walisema kuwa serikali ya kaunti hiyo inafaa kuanzisha hazina ya kaunti ambayo ni ya kina mama pekee ili kuwasaidia kujiendeleza na kujikimu kimaisha haswa kwa kufanya biashara.

“Wakati tunapokezwa pesa kupitia vikundi hazitutoshi, tunaomba serikali ya kaunti kututengea sisi kina mama pesa zetu kwa kutuanzishia hazina yetu,” alisema Moraa.

Aidha, Mary Kerubo, mwanabiashara mwingine alisema kina mama wanahitaji kuinua uchumi wa kaunti na taifa kupitia biashara,  na kusema kuna haja yao kutengewa hazina yao ili kufanya biashara zao kikamifu.