Serikali ya kaunti ya Kisii imeombwa kujali afya ya wakazi wa kaunti hiyo ili kutoathirika na magonjwa mbalimbali.
Wito huo umetolewa baada ya uchafu wa taka za kila aina kutupwa katika eneo la Ogembo bila wakazi wa eneo hilo kujulishwa
Wakizungumza siku ya Jumapili katika eneo hilo, wakazi wa kijiji cha Kanyimbo na Nyatuga, karibu mahala uchafu huo unatupwa, wakazi hao walilalamikia uchafu huo, huku wakiomba serikali ya kaunti hiyo kutafuta mahala tofauti pa kutupa uchafu.
Aidha, walisema watoto wao wameathirika pakubwa, huku mmoja wao akisema amewapeleka wanawe hospitalini ili kuangaliwa kutokana na kusumbuliwa na tumbo.
“Hatujui ni nani aliruhusu uchafu kuanza kutupwa katika eneo hili penye tunaishi, maana hatukuhusishwa ili tukubali au tukatae,” alisema Dennis Ontita, mmoja wa wakazi.
“Tunaomba serikali ikome kuweka uchafu huu hapa na kutafuta mahali pengine, au kununua shamba ambapo watu hawaishi maana harufu ambayo inatoka katika eneo hili ni mbaya zaidi,” alisema Peterson Maiko, mkazi mwingine.