Serikali ya kaunti ya Mombasa imeshinikizwa kuhakikisha kuwa inarekebisha mabomba ya maji taka ili kuhakikisha kuwa wazuia mafuriko katika kaunti hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Watalii nchini yaani Bi Milicent Adhiambo amesema kuwa kushuhudiwa kwa mvua nyingi mjini Mombasa huenda kukasababisha hasara kubwa iwapo mitaro hiyo haitarekebishwa kwani hata sekta ya utalii itaathirika pakubwa.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Adhiambo amesema kuwa mara nyingi mji wa Mombasa hujaa taka nyingi zinazosombwa na maji taka na kuharibu sifa ya mji huo ambao ni kati ya vivutio vya utalii kanda ya Pwani.
"Serikali ya kaunti ya Mombasa kupitia idara ya mazingira inafaa ihakikishe kuwa inahifadhi hadhi ya mji wa Mombasa kwa kuweka mazingira safi na kurekebisha mabomba ya maji taka ili kuhakikisha kuwa sekta ya utalii haikumbwi na changamoto hasa msimu huu wa mvua," alisema Adhiambo.
Kauli yake inajiri huku mji wa Mombasa ukijaa mirundiko ya taka zilizosombwa na maji taka pamoja na mafuriko yakianza kushughudiwa mjini humo.