Mwenyekiti wa hospitali ya Kiogoro iliyoko eneo bunge la Nyaribari Chache kaunti ya Kisii Meshack Anunda ameomba serikali ya kaunti hiyo kuwalipa wahudumu wa afya pesa zao walizofanyia kazi.
Kulingana na Anunda, aliyezungumza na mwanahabari huyu alisema wahudumu wa afya katika hosptali hiyo ambao wako saba hawajalipwa pesa zao tangu mwezi wa nane mwaka jana, huku wakiahidiwa kulipwa pesa hizo kwa muda mrefu.
Anunda alisema huduma katika hospitali hiyo zimelemazwa pakubwa kufuatia ukosefu wa mishahara kwa wahudumu wa afya, jambo ambalo limewakera na kuomba serikali kuwajali na kuwalipa pesa zao ili huduma za matibabu kuendelea bila changamoto yoyote.
“Wahudumu wa afya katika hospitali hii ya Kiogoro hawajalipwa pesa zao, lakini maafisa wa kaunti waliahidi kutulipa, ahadi ambayo haijatimia hadi sasa,” alisema Anunda.
Ikimbukwe kuwa juma lililopita wahudumu hao waliomba serikali kuwaunganishia nguvu za umeme ambazo zilikatishwa Desemba mwaka jana kufuatia ukosefu wa pesa, huku hospitali hiyo ikiendelea kusalia gizani.