Serikali ya kaunti ya Kisii imehimizwa kutoa usaidizi kwa shule za walemavu katika kaunti hiyo ili kuinua viwango vya elimu katika shule hizo.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa shule hizo hazipati usaidizi wa kutosha kama shule zingine jambo ambalo hurudisha elimu nyuma katika shule hizo.
Akizungumza siku ya Jumapili katika shule ya walemavu ya Giachere Friends, mwalimu mkuu wa shule hiyo Rose Obinchu aliomba serikali ya kaunti ya Kisii kusaidia shule za aina hiyo kifedha na mahitaji mengine ya kimasomo ili kujiendeleza zaidi.
Pia mwalimu huyo alisema wanafunzi wa shule hizo wanastahili kupokea usaidizi katika kitengo cha michezo kwani hajabobea katika upande huo kufuatia ukosefu wa pesa za kuwawezesha kujiendeleza.
“Tunaomba serikali ya kaunti kusaidia shule za walevu ili viwango vya masomo katika shule hizo kuinuka zaidi kutoka mahali zilipo kwa sasa,” alisema Obinchu.
Wakati huo huo, mwenyekiti wa muungano wa vijana katika kaunti ya Kisii, almaarufu Kisii Youths Alliance, Esther Okenyuri aliomba wabunge na wawakilishi wadi pamoja na serikali ya kitaifa kuwa katika mstari wa mbele kusaidia watoto ambao hawajiwezi haswa mayatima na wa familia maskini ili kujiendeleza kielimu.