Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amesema kwamba serikali yake imeandikisha mkataba na kampuni ya Magari na Pikipiki Honda ili kuiuzia serikali ya kaunti ya Nyamira pikipiki mia 300, pikipiki zitakazopokezwa baadhi ya wahudumu wa pikipiki katika kaunti hiyo ili kujiendelesha.
Akihutubia wakazi wa Magwagwa kwenye eneo bunge la Mugirango kaskazini wakati wa kutembelea miradi mbalimbali siku ya Jumatatu, Nyagarama alisema kuwa tayari serikali yake imekubaliana na kampuni ya Honda kuhusiana na ununuzi wa pikipiki hizo.
"Tayari serikali yangu imeweka mikakati yakununua pikipiki mia 300 kutoka kwa kampuni ya Honda ili kuwapokeza vijana wetu walio na nia ya kujistawisha na tumekubaliana na kampuni hiyo kulipa pesa nusu kisha vijana watakaonufaika walipie pesa zilizosalia kama mikopo kupitia kwa Sacco zao," alisema Nyagarama.
Nyagarama aidha aliongeza kwa kuwahimiza wahudumu wa pikipiki kujiunga na Sacco ikiwa wangependa kunufaika na mpango huo.
"Ukweli ni kwamba watakaonufaika kutokana na mpango huu ni wahudumu wa pikipiki walioko kwenye vyama vya kujistawisha na ndio maana nawahimiza wale ambao wangali kujiunga na Sacco kufanya hivyo kwa haraka," aliongezea Nyagarama.
Picha: Gavana Johna Nyagarama katika hafla ya hapo awali. Amesema kuwa serikali yake imeingia katika mkataba na kampuni ya Honda ili kuwafaidi vijana wa eneo hilo. WMaina/Hivisasa.com