Baadhi ya wakaazi wa Nyamache katika eneo Bunge la Bobasi wameipongeza Serikali ya Kaunti ya Kisii kwa kuinua viwango vya huduma katika hospitali ya Nyamache.
Wakiongea siku ya Alhamisi na mwaandishi huyu katika hospitali ya Nyamache, wakazi hao walimpongeza Gavana James Ongwae kwa kuboresha huduma katika hospitali hiyo haswa kwa kuwepo kwa mashine ya kutumika katika upasuaji.
Haya yanajiri wakati serikali ya kaunti ya Kisii, kupitia sekta ya afya kuazisha mradi wa kusaidia hospitali za kitengo cha nne ili kuinua viwango vya hudumu katika hospitali hizo.
"Napongeza Serikali ya Kaunti yetu ya Kisii kwa kutukumbuka na kutusaidia katika hospitali hii ili nasi tuweze kunufaika na huduma bora ya afya," alisema Jeremia Isoe, mkazi.
Wakazi hao walisema kuwa kutokana na kuongezwa kwa madktari wawili, sasa wana matumaini kuwa watasaidika pakubwa kwa kuwa hospitali hiyo imekuwa na daktari mmoja ambaye hakuwa anaweza kuwatibu wagonjwa wote.
"Tumekuwa na shida kubwa kwa kuwa tulikuwa na daktari mmoja lakini kwa sasa hatuna shida hiyo tena kwani tumepata daktari wengine wawili na natumai kuwa tutapata kuhudumiwa vizuri," alisema Silwel Ochong’a, mkazi.
Wakazi hao walisema sasa watapata matibabu katika hospitali hiyo bila kulazimika kuenda katika mji wa Kisii kutafuta matibabu kama hapo awali kwani hospitali hiyo ina vifaa vinanavyoitajika kwa huduma ya afya.