Wanawake wajawazito katika Hospitali ya Junda huko Mishomoroni wameipongeza hatua ya viongozi wa kaunti kutoa vifaa vya kiafya ikiwemo ambulensi nne kwa hospitali hiyo.
Wakizungumza walipokuwa kwenye hospitali hiyo, kina mama hao walisema kuwa itakuwa rahisi kwao kusafiri hadi hospitali haswa ikizingatiwa kuwa madaktari wa nyanjani walio chini ya mpango wa 'Plan International' wataweza kuwasiliana na hospitali hizo moja kwa moja endapo kunahijatika huduma za dharura.
Wanawake hao walisema kuwa wamekuwa wakipata changamoto ya kufika hospitalini wanapokaribia muda wa kujifungua, na kusema kuwa ambulensi hizo zitarahisisha usafiri wao.
Lucy Kalekya, alisema kuwa pia itakuwa rahisi kwao kusafirishwa hadi katika Hospitali kuu ya Pwani iwapo watahitaji matibabu zaidi.
Margaret Zani, ambaye ni mkunga katika hospitali hiyo, alipongeza hatua hiyo ya serikali ya kaunti kwa kusema kuwa itachangia katika kupunguza visa vya wanawake wajawazito kufariki kabla ya kufikishwa hospitali.
Aidha, alisema kuwa wagonjwa wanaougua nyakati za usiku pia watanufaika pakubwa na huduma hiyo.
Gavana Hassan Joho, Mbunge wa Kisauni Rashid Benzimba pamoja na mwakilishi wa kina mama Mishi Mboko waliongoza hafla hiyo ya kutoa ambulensi nne kwa Hospitali ya Junda.