Mwakilishi mteule kwenye bunge la kaunti ya Nyamira Zipporah Osoro amejitokeza kumtaka mwenyekiti wa kamati ya usimamizi wa umma James Mating'a kuweka mikakati ya kuhakikisha bodi ya kuajiri wafanyakazi inaajiri walimu zaidi walio na ulemavu kwenye shule za chekechea.
Akichangia kwenye hoja ya kutaka kujua idadi ya walemavu ambao wameajiriwa na serikali ya kaunti hiyo siku ya Jumanne, Osoro alisema yafaa Mating'a ashawishi bodi ya kuajiri wafanyakazi ili itenge nafasi za kuajiri walimu walemavu.
"Ikiwa wewe ni mwenyekiti wa kamati ya usimamizi wa umma kwenye bunge hili ni jukumu lako kuhakikisha kuwa walimu wa shule za chekechea hasa wale walio na ulemavu wanaajiriwa na bodi ya kuajiri wafanyakazi humu Nyamira," alisema Osoro.
Osoro aidha alihimiza bunge la kaunti hiyo kuidhinisha miswaada inayotetea maslahi ya walemavu katika jamii.
"Ili haki za watu wanaoishi na ulemavu ziheshimiwe, sharti tuhakikishe kama bunge kwamba tunaidhinisha sheria zitakazo tetea maslahi yao," aliongezea Osoro.