Mbunge wa Nyali ameihimiza serikali ya Kaunti ya Mombasa kubuni miradi mbalimbali itakayowawezesha wachuuzi katika kaunti hiyo kujiendeleza kibiashara.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Hezron Awiti alisema iwapo serikali ya kaunti italiangazia swala hilo, basi maswala ya uhalifu na utumizi wa mihadarati miongoni mwa vijana yatapungua kwa kiasi kikubwa.
Awiti amemtaka Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho pamoja na baraza lake la wakuu wa idara mbali mbali kuhakikisha kuwa maswala kama hayo yanapewa kipau mbele.
"Tunaitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kuwatengea vijana hasa wachuuzi nafasi za miradi ili kufanya biashara zao kikamilifu,” alisema Awiti.
Aidha, mbunge huyo ameikosoa serikali ya kaunti kwa madai ya kushindwa kumudu gharama ya maisha ya wakaazi, kutokana na kupandishwa kwa ushuru unaotozwa wafanyibiashara pamoja na bidhaa zingine muhimu.