Serikali ya Kaunti ya Mombasa imetia saini mkataba wa makubaliano na chuo kikuu kimoja kutoka nchini Malaysia, kwa lengo la kusaidia wanafunzi kutoka eneo hilo.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Usimamizi wa chuo cha Management and Science University (MSU) umeahidi kusaidia vyuo vikuu katika Kaunti ya Mombasa na Pwani kwa ujumla katika mambo tofauti ikiwemo kutoa ufadhili wa masomo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kutia saini mkataba huo, Rais wa chuo hicho Dkt Mohamed Shukri alishauri taifa la Kenya kuwekeza zaidi katika elimu hasa ya kimataifa.

“Lazima taifa liwekeze katika elimu ili liweze kuwa dhabiti. Hatua hii itasaidia kuinua viwango vya maisha hasa katika jamii za watu wasiojiweza,” alisema Shukri.

Katika mkataba huo, chuo cha MSU kimejitolea kuleta wataalam wa elimu na sayansi kutoka nchini Malaysia ili kushirikiana na vyuo hivyo katika vitengo mbalimbali.

Vile vile, kutakuwa na ushirikiano wa karibu katika shughuli za kufanya utafiti wa kisayansi miongoni mwa vyuo hivyo, ambapo wanafunzi kutoka Kenya watakuwa wakipewa ufadhili kwenda Malaysia kwa masomo zaidi.

Mkuu wa Idara ya Elimu Kaunti ya Mombasa Tendai Lewa, kwa upande wake amesema hatua hiyo ni kutokana na juhudi za serikali hiyo za kutafuta msaada kutoka kwa mataifa ya nje.

“Tumezunguka mataifa kama vile Uingereza, Marekani, Japani na kadhalika. Tunashukuru Malaysia wamekuwa wa kwanza kuitikia wito huu na tunasema kwamba hili ni tukio la kihistoria kabisa,” alisema Tendai.

Mkataba huo pia unatarajiwa kusaidia mradi wa kimataifa wa kutoa ufadhili kwa wanafunzi mjini Mombasa maarufu kama 'Governors Award International Programme'.