Serikali ya Kaunti ya Mombasa imetia saini mkataba na usimamizi wa Chuo cha mafunzo ya matibabu nchini KMTC.
Mkataba huo unatarajiwa kuwawezesha wanafunzi wengi kusomea taaluma hiyo bila ya vikwazo.
Akiongea katika hafla ya maonyesho ya mafunzo yanayotolewa chuoni humo mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir alisema mipangilio tayari imewekwa ili kuhakikisha idadi kubwa ya vijana wa Kaunti hiyo wanasajiliwa katika vyuo hivyo kusomea taaluma ya matibabu.
Nassir alisema ni sharti vyuo hivyo viwatambue vijana walio katika eneo la Pwani.
Aidha, aliema kuwa wahudumu wa afya kwenye jamii pia watafadhiliwa ili waongeze ujuzi wao.
“Tumetia saini mkataba utakaohakikisha kuwa wanafunzi wanasomea taalum mbalimbali za kimatibabu bila pingamizi na kufanikisha maswala ya afya kwa jamii mashinani,” alisema Abdulswamad.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wadi ya Tudor Patrick Simiyu alisema kuwa vijana wa Kaunti ya Mombasa wanafaa kupata elimu ya kutosha, ili waweze kujitenga na maovu.
Hafla hiyo ya kuhamasisha umma kuhusiana na taaluma za matibabu na mafunzo mengine yanayotolewa katika chuo hicho pia iliandaliwa katika katika chuo hicho, tawi la Port Reitz eneo la Changamwe.