Serikali ya Kaunti ya Mombasa imetangaza kukabiliana na mkurupuko wa maradhi ya kipindupindu katika kaunti hiyo.
Mkuu wa Idara ya Afya katika Kaunti ya Mombasa Mohamed Abdi alisema kuwa tayari mikakati ya kuzuia kuenea kwa maradhi hayo katika Kaunti ya Mombasa inatekelezwa, huku akisema kuwa hospitali zote pamoja na zahanati zimejiandaa kuzuia kuchipuka kwa maradhi hayo.
Akizungumza na wanahabari baada ya kuzuru Hospitali kuu ya ukanda wa Pwani mjini Mombasa siku ya Jumanne, Abdi alisema kuwa zaidi ya kesi 21 zimeripotiwa na waathiriwa wanaendelea kupata matibabu katika hopsitali hiyo.
Aliongezea kuwa hakuna mtu hata mmoja aliyeripotiwa kuaga dunia.
"Tumapata ripoti za kuchipuka kwa mkurupuko wa maradhi ya kipindupindu katika eneo letu lakini waathiriwa tayari wanaendelea kupokea matibabu na tunamatumaini watapata nafuu. Hatahivyo, mikakati imeandaliwa kuzuia kuenea kwa maradhi hayo,” alisema Abdi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mkuu wa Idara ya Afya katika Kaunti ya Mombasa Dkt Khadijah Shikelli aliwahimiza wakaazi kuzingatia mazingira safi sambamba na kutumia maji safi ili kuepukana na maradhi hayo.
Haya yamejiri baada ya Wizara ya Afya nchini kutangaza kuchipuka kwa mkurupuko wa maradhi ya kipindupindu hasa msimu huu ambapo Wakenya wanatarajia mvua nyingi.
Wizara hiyo imewataka Wakenya kuwa waangalifu sawa na kuzingatia usafi wa mazingira na utumizi wa maji safi.