Idara ya afya katika Kaunti ya Mombasa imesema kuwa imeanzisha zoezi la kusambaza neti kwa wakaazi kama njia ya kuzuia kuchipuka kwa maradhi ya ugonjwa wa chikungunya, yanayosababishwa na mbu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Jumanne, mkuu wa idara ya afya Kaunti ya Mombasa, Mohammed Abdi, alisema kuwa zoezi hilo tayari limetekelezwa katika maeneo ya Kisauni, Mwakirunge na Junda, huku maeneo ya Likoni na Changamwe pia yakilengwa.

“Mombasa inapokea wageni kutoka maeneo mbalimbali nchini na hata kutoka ugaibuni. Hivyo kama serikali ya kaunti, tumechukua hatua ili kuwalinda wananchi wetu,” alisema Abdi.

Aidha, Abdi alitoa wito kwa wananchi kupiga ripoti kwa idara ya afya ya kaunti iwapo watashuhudia kuenea kwa mbu katika maeneo yao ya makaazi, ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.

Kulingana na ripoti iliyotolewa siku ya Jumatatu na taasisi ya kufanya utafiti kuhusu madawa nchini KEMRI, maeneo ya Mombasa na Kusini mwa Kenya yapo kwenye hatari ya kukumbwa wa Chikungunya kutokana na joto jingi.

Eneo la Mombasa liilikumbwa na ugonjwa wa Chukungunya mwaka 2004.