Naibu kaunti kamishna wa kaunti ndogo ya Rabai Wilfred Sigei amezitaka kauti za Pwani kutatua tatizo la ubadhirifu wa fedha zilizotengwa kuwasaidia wasiojiweza katika jamii.
Akizungumza huko Kadzuyuni Rabai, Sigei amesema kwamba japo serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa wazee wanapata malipo yao ya kila mwezi, kumekuwepo na ongezeko la malalamishi ya utumizi mbaya wa fedha hizo miongoni mwa kaunti mbalimbali hapa Pwani na hata kutumika kinyume na mipango ya serikali.
Kulingana na Sigei ni kuwa waliopewa jukumu la kuwasaidia wazeee katika jamii kupata malipo yao ya kila mwezi wamefeli kutekeleza wajibu wao kwani mara nyingi fedha hizo huonekana kurudishwa katika akaunti za serikali huku akisema kuwa wazee wengi vijijini hawajui wakati wa kwenda kuchukua fedha zao kauli ambayo iliungwa mkono na wawakilishi wa wadi mbalimbali waliohudhuria mkutano huo.
Sigei aidha ameongeza kuwa hivi karibuni wataanzisha uchunguzi ili kubaini anayefaidika na fedha hizo ambazo serikali kuu imetengea wazee huku akiseema kuwa huenda ikawa serikali za kaunti zinatumia fedha hizo vibaya kutokana na wazee haswa maeneo ya mashinani kutoshirikishwa katika mipango ya serikali za Kaunti.
Kwa upande wa wanafunzi wasiojiweza Sigei amesema kwamba kumekuwepo na mikakati ya kuwasidia wanafunzi hao lakini baadhi ya fedha ambazo serikali imekuwa ikiwatengea zimeishia mikononi mwa wakuu kwenye Kaunti mbalimbali hapa Pwani jambo ambalo amelitaja kama kurudisha nyuma viwango vya elimu miongoni mwa Kaunti za Pwani.
Hata hivyo amezitaka Kaunti zote kanda ya Pwani kuweka mikakati madhubuti ili kuona kwamba wanaofuja fedha hizo wanatambulika na hatua dhidi yao kuchukuliwa mara moja.