Seneta wa Kaunti ya Mombasa Hassan Omar ameshutumu viwango vya kodi vinavyotozwa wafanyabiashara humu nchini.
Seneta huyo amesema utozaji wa kodi za juu katika serikali za kaunti umewanyima wananchi nafasi ya kujistawisha kibiashara na pia kuregesha nyuma uwekezaji.
Akizungumza katika kongamano la muungano wa sekta za kibinafsi na maseneta linaloendelea jijini Mombasa, Omar alisema kuwa hatua hiyo inawafanya wananchi kutonufaika na serikali za ugatuzi.
“Tumefanya biashara ndogo ndogo kama za mama mboga kuwa ngumu. Hii ni kwa sababu ushuru tunaotoza ni wa juu zaidi kulinganisha na biashara yenyewe. Lazima tuupunguze ushuru ili kufanikisha biashara na kuwapa watu waojihusisha na biashara ndogo ndogo nafasi,” alisema Omar.
Omar alilalamika kuwa fedha zinazotozwa kama ushuru kutoka kwa wafanyabiashara hao huishia katika miradi ya kaunti isiyokuwa na manufaa kwa mwanachi wa kawaida.
Aidha, amesititiza kuwa ushuru unaotozwa katika mipaka ya kaunti moja hadi nyingine pia ni changamoto kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara katika kaunti anuai humu nchini.
"Mfanyabiashara anayetoka Kilifi akifika Mombasa analipa ushuru, anapoondoka Mombasa kueleka kwale analipishwa tena. Kaunti ya Machakos bado inamsubiri kumtoza ushuru, kabla ya Kaunti ya Nairobi kumalizia kuchukua ushuru,” alisema Omar.
Hata hivyo, Seneta huyo alisema kuwa watafanya majadiliano wakiwa na nia ya kurekebisha sheria zinazowakandamiza wawekazaji kote nchini.