Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Kwale ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa baraza la magavana nchini Salim Mvurya amemtaka waziri mpya wa madini Dan Kazungu kuhakikisha kuwa sekta hiyo inaimarika na kufaidi zaidi Wapwani.

Gavana huyo amemtaka waziri huyo kujitahidi vilivyo ili kuona kwamba Wapwani wanafaidi kutokana na utajiri wa raslimali walionao katika eneo hilo.

Alikuwa akiongea hayo siku ya Ijumaa wakati waziri huyo alipofanya ziara ya kwanza katika kaunti hiyo tangu alipoteuliwa kama waziri ambapo walifanya mazungumzo na gavana huyo.

“Tunamtaka waziri wetu wa madini mabaye tayari ameanza kazi yake kuhakikisha kwamba anaweka mikakati ili kaunti zetu zinufaike na madini ambayo tuko nayo pamoja na jamii zetu kwa ujumla,” alisema Mvurya.

Kwa upande wake waziri Kazungu ambaye pia anatokea Pwani eneo la Malindi aliahidi kwamba atazingatia zaidi katiba inavyosema kuhusu masuala ya madini ili wananchi wanufaike.

“Sheria mpya ya kuhusu madini inatarajiwa kuanza kufanya kazi katika kipindi cha miezi 3 ijayo na itazingatia sana ugawaji sawa wa raslimali miongoni mwa wakenya wote,” alisema Waziri.

Eneo la Pwani linafahamika zaidi kuwa na utajiri mkubwa wa madini lakini wakaazi kwa muda wamekuwa wakilalama kwamba hawafaidiki vilivyo kutokana na madini hayo.

Kaunti ya Taita-Taveta ikisifika kwa uchimbaji wa madini mbalimbali, huku Kaunti ya Kwale ikiwa kaunti ya kipekee nchini inayotoa madini aina ya Titanium yanayosafirishwa kupitia bandari ya Mombasa hadi mataifa ya ng’ambo.

Hata hivyo Wapwani wengi walifurahishwa na uteuzi huo wa aliyekuwa mbunge wa Malindi Dan Kazungu kuwa waziri mpya wa madini wakiwa na matumaini kwamba tatizo lao la mika mingin litaweza kutatuliwa.