Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) limewasilisha kesi katika Mahakama kuu jijini Mombasa dhidi ya gavana wa Mombasa pamoja na mawaziri wawili.

Share news tips with us here at Hivisasa

Haya yanajiri kufwatia mtafuruku wa kipande cha ardhi unaohusisha pande zote mbili.

Shirika hilo likiongozwa na wakili Saende Protus limeitaka mahakama kuwahukumu gerezani Gavana Hassan Joho, Katibu wa serikali ya Kaunti Mombasa Francis Thoya, na mkuu wa Idara ya Ardhi Anthony Njaramba, kwa madai ya kupuuza uamuzi uliotolewa na Jaji Anne Omollo mnamo Aprili 27, 2016.

Uamuzi huo uliruhusu KBC kuezeka uwa katika kipande hicho cha ardhi.

Hatua hii inajiri wiki chache baada ya Gavana Joho kuongoza vijana katika kubomoa ukuta uliozunguka ardhi hiyo inayozozaniwa.

Upande wa mashtaka umewasilisha stakabadhi mahakamani kama sehemu ya ushahidi katika kesi hiyo, ikiwemo barua rasmi iliyoandikwa na mkurugenzi wa KBC kumuarifu mkuu wa Idara ya Ardhi kuhusu kujengwa kwa ukuta huo katika ardhi hiyo iliyoko katika eneo la Nyali.

Aidha, wakili Saende ameiomba mahakama kuwaamuru washtakiwa kulipa shilingi 1,980,000 pesa inayoripotiwa kugharamia ujenzi wa ukuta huo.

Jaji Anne Omollo amempa wakili wa upande wa washtakiwa muda wa siku 21 kujiandaa kujibu madai hayo.

Kesi hiyo inatarajiwa kusikizwa mnamo Novemba 17, 2016.