Mbunge wa Bomachoge Chache kaunti ya Kisii Simon Ogari ametofautiana vikali na muungano wa upinzani Cord dhidi ya kuwaondoa wanajeshi nchini Somalia na kusema wanajeshi hao wataendelea kusalia nchini humo.
Akizungumza katika mazishi ya mwanajeshi aliyeuawa kwenye shambulizi la al-Shabaab eneo la Ogembo kaunti ya Kisii, Ogari alisema hakuna vile wanajeshi wataondoka Somalia ila watapambana na al-Shabaab hadi mwisho.
Ogari alikosoa Cord kwa kuhitaji serikali ya Kenya kuwaondoa wanajeshi hao kwa kuhofia mashambulizi ya mara kwa mara huku akisema liwe liwalo wanajeshi wataendelea kukabiliana na al-Shabaab kuhakikisha visa vya ugaidi vimesitishwa nchini humo.
“Wanajeshi wa Kenya wataendelea kukabiliana na magaidi wa al-Shabaab hadi mwisho na hakuna vile wataondolewa na ninaomba Cord iwachene na fikra kama hizo ili taifa letu lizidi kupambana na magaidi,” alisema Ogari .