Maafisa kutoka Halmashauri ya ukadiriaji ubora wa bidhaa nchini KEBS wamefunga kampuni tano za maji ya chupa katika Kaunti ya Mombasa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kulingana na taarifa ya Halmashauri hiyo, kampuni hizo zikiwemo ile ya Bamba iliyo katika eneo la Nyali, Zeit katika eneo la Kisauni, Zahra cool iliyo katika maeneo ya Ganjoni, Sundus ikiwa katika eneo la Majengo na ile ya Active iliyo katika eneo la Bombolulu Mjini Mombasa zimefungwa kufuatia bidhaa hizo kutiliwa shaka.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Afisa mkuu wa Halmashauri hiyo Martin Nyakiomo, amesema kuwa kampuni hizo zimekuwa zikiweka maji kwenye chupa na kuwauzia watu bila ya idhini kutoka kwa KEBS hivyo basi bidhaa hiyo kutokuwa safi kwa matumizi ya mwanadamu.

"Tumepata ripoti kutoka kwa wakaazi kuwa baadhi ya kampuni mjini Mombasa zinatengeza maji ya chupa bila idhini rasmi kutoka kwa Halmashauri na tumechukua jukumu hilo la kuhakikisha tumezifunga na atakayepatika atachukuliwa hatua za kisheria," alisema Martin. 

Shirika hilo limesema kwamba uchunguzi zaidi kuhusiana na kampuni zinazoweka maji kwenye chupa katika kaunti hiyo ya Mombasa ungali unaendelea na kampuni ambazo hazijatimiza viwango hitajika vya usafi wala usalama kwa bidhaa zao zitafungwa.

Hatua hiyo inafuatia mkurupuko wa maradhi ya Homa nyongo katika kaunti ya Mombasa, mkurupuko ambao umechangiwa na unywaji wa maji chafu miongoni mwa wakaazi.