Shirika la ukadiriaji ubora wa bidhaa nchini KEBS limetakiwa kuanzisha uchunguzi mara moja kuhusu makampuni ya maji yanayodaiwa kuuza maji ya chupa yasiyokuwa salama kwa matumizi ya binadamu.
Kulingana na chama cha maendeleo ya wanawake katika kaunti ya Mombasa, swala hilo la utumizi wa maji chafu katika Kaunti ya Mombasa limefikia viwango vya kutisha kwa sasa na ni lazima likabiliwe vilivyo la sivyo wakaazi watapoteza maisha yao kufuatia mkurupuko wa maradhi ya homanyongo.
Katika mkao na wanahabari katika afisi za chama hicho mjini Mombasa siku ya Jumatano, mwenyekiti wa chama hicho katika kaunti ya Mombasa Afiya Rama amesema kwamba shirika hilo halina budi ili kuidhinisha uchunguzi wa kina dhidi ya makampuni hayo ili kuwahakikishia wakaazi wa kaunti hiyo ya Mombasa usalama wa maji wanayotumia kila uchao.
Afiya ameikosoa kampuni ya usambazaji maji ya Kaunti hiyo ya Mombasa kwa kushindwa kuboresha huduma za maji na kusababisha uhaba mkubwa wa maji katika kaunti hiyo hali iliyowalazimu wakaazi kutumia maji ya kisima ambayo sio salama kwa afya ya binadamu.
"Tunashangazwa na kampuni ya kusambaza maji Mombasa imeshindwa kabisa kuwajibikia majukumu yake na kusababisha uhaba wa maji kila mara na hatua hiyo ndio imechangia kukithiri kwa kampuni nyingi za kutengeza maji ya chupa zisizoidhinishwa kikatiba," alisema Afiya.
Hofu ya wanawake hao inajiri baada ya wizara ya afya katika Kaunti hiyo ya Mombasa kukiri kwamba visa vya maambukizi ya homanyongo yaani Hepatitis A vimeongezeka kutoka 21 hadi 114 katika kipindi cha juma moja pekee hali ambayo imewatia hofu wakaazi katika kaunti hiyo.