Kampuni ya KenGen imezindua mradi wa uzalishaji kawi wa shilingi bilioni 29 ili kuwezesha usambazaji wa nguvu za umeme nchini kwa kasi zaidi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo imesema kuwa tayari serikali imeahidi kutoa shilingi bilioni 20 kufanikisha shughuli hiyo itakayowasaidia Wakenya wengi kupata nguvu za umeme hadi mashinani.

Mkurugenzi mkuu wa bodi ya kampuni hiyo Albert Mugo amesema kuwa mradi huo utaanza hivi karibuni huku akiwahimiza wadau wa sekta mbalimbali za kawi kushirikiana na kampuni hiyo kufanikisha mradi huo.

"Tayari tuna mipango ya kuzalisha kawi zaidi ili kuhakikisha kuwa wakaazi mashinani wanapata umeme. Pesa tayari zimetolewa na serikali kushughulikia swala hilo,” alisema Mugo alipokuwa akiwazungumzia wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne.

Wakurugenzi wa bodi ya kampuni hiyo wanatarajiwa kukutana na Gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Joho kwa mazungumzo kuhusu jinsi mradi huo utakavyotekelezwa kutoka Naivasha hadi mjini Mombasa.

Wakurugenzi wa bodi hiyo pia watatembelea maeneo mbalimbali katika Kaunti ya Mombasa ili kufanya ukaguzi kabla ya mradi huo kuanza rasmi.