Huenda changamoto zinazopitiwa na wakaazi katika kivuko cha feri cha Likoni zikasitishwa baada ya Mamlaka ya barabara kuu nchini KeNHA, kutangaza mpango wa ujenzi wa daraja katika kivuko cha feri cha Likoni.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo Peter Mundinia, amesema kuwa mipango ya ukaguzi katika eneo hilo unaendelea ili kutambua jinsi shughuli hiyo ya ujenzi wa daraja itafanyika bila ya kuwafurusha wakaazi katika ardhi zao.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Mundinia alisema kuwa mamlaka hiyo itawahusisha wakaazi katika vikao vya maoni ili kuhakikisha kuwa shughuli hiyo inafanyika kwa makubaliano na wakaazi wa eneo hilo.

Aidha, alisema kuwa ujenzi huo unatarajiwa kusitisha changamoto za msongamano katika kivuko hicho.

Aidha, alisema kuwa ujenzi huo unatarajiwa kuanza baada ya kipindi cha mwaka mmoja wa ukaguzi na madajiliano baina ya wakaazi na washauri wa miradi nchini, ili ujenzi huo kufanywa bila ya vizuizi.

"Tayari mipango ya ujenzi wa daraja katika kivuko cha feri cha Likoni inaendelea na hivi karibuni ujenzi huo utaanza baada ya wakaguzi kumaliza shughuli zao pamoja na kuwahusisha wakaazi katika kutoa maoni,” alisema Mundinia.

Kivuko cha feri cha Likoni hushuhudia msongamano wa wakaazi kutokana na hitilafu zinazokumba feri mara kwa mara.