Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wadau wa sekta ya uchukuzi mjini Mombasa wamelalamikia kukithiri kwa misongamano ya magari ya uchukuzi katika eneo la Kibarani na Jomvu katika Kaunti ya Mombasa.

Wadau hao walisema kwamba msongamano unaoshuhudiwa katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi hususan katika maeneo ya Kibarani na Jomvu umechangia pakubwa hasara kutokana na kucheleweshwa kwa mizigo inayosafirishwa kutoka bandari ya Mombasa.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Katibu wa chama cha wachukuzi wa masafa marefu cha ‘Trackers union’ Ahmed Omar, alisema kwamba hali hiyo hutatiza shughuli za uchukuzi hususan pindi kunapotokea ajali.

“Misongamano ya mara kwa mara katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi hususan katika eneo la Kibarani na Jomvi imeathiri pakubwa shughuli za usafirishaji wa mizigo kutoka kwa bandari ya Mombasa,” alisema Omar.

Omar ameitaka halmashauri ya barabara kuu nchini KENHA kuibuka na mbinu itakayoidhibiti misongamano ya mara kwa mara katika eneo hilo huku akiishinikiza Serikali ya kaunti ya Mombasa na Idara ya trafiki kulishughulikia tatizo hilo.

“Tunaiomba halmashauri ya barabara kuu nchini KENHA kubuni njia mbadala za kuimarisha shughuli za usafiri hususana magari ya masafa marefu ili kupunguza msongamano ya mara kwa mara barabarani,” aliongeza Omar.

Lalama za wadau hao zinajiri baada ya ajali zinazotokea katika eneo la Kibarani kusambaratisha shughuli za uchukuzi kati ya maeneo ya Changamwe na katikati mwa mji la Mombasa.