Msongamano unaoshuhudiwa mara kwa mara katika kivuko cha feri cha Likoni huenda ukafika kikomo baada ya kampuni inayotoa huduma za feri nchini Kenya Ferry Services kutangaza azma ya kuzindua upya kivuko cha feri cha Mtongwe.
Kaimu mkurugenzi wa kampuni ya huduma za feri Bakari Khamis Gowa alisema kwamba kivuko hicho hutumiwa na zaidi ya watu elfu 20 kila siku hivyo basi kivuko cha Mtongwe kitapunguza msongamano.
Akizungumza na wanahabari katika afisi za Shirika hilo mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Gowa alisema kwamba wanatarajia feri mbili mpya humu nchini Disemba mwaka huu na feri moja itatoa huduma katika kivuko cha Mtongwe.
“Tunatarajia kupata feri mbili mwishoni mwa mwaka huu na moja itahudumu katika eneo la Mtongwe kupunguza msongamano katika kivuko cha Likoni,” alisema Gowa.
Shughuli za uchukuzi katika kivuko hicho cha feri zilisitishwa takriban miaka saba iliyopita baada ya eneo la kuegesha feri kubomoka.