Mkurugenzi wa Chuo cha mafunzo ya matibabu cha KMTC amesema kuwa Kenya ina upungufu wa jumla ya wauguzi elfu 26.
Peter Tum amesema kuwa licha ya serikali kuwekeza katika sekta ya afya iliyo chini ya serikali za ugatuzi, vyuo vya mafunzo ya matibabu vina sajili idadi ndogo ya wanafunzi wanaojiunga na taasisi hizo.
Alisema kuwa jumla ya wanafunzi elfu 26 hutuma maombi ya kujiunga na vyuo hivyo kila mwaka lakini elfu tisa pekee ndio wanaosajiliwa.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika ufunguzi rasmi wa jengo la madarasa katika Chuo cha mafunzo ya matibabu cha KMTC tawi la Mombasa, Tum alisema kuwa licha ya kuwepo kwa upungufu huo wa wauguzi, kuna idadi kubwa ya wauguzi waliondoka nchini kuelekea katika mataifa ya nje kufanya kazi.
“Tunavyozungumza sasa kuna upungufu wa takriban wauguzi elfu 26 kote nchini. Hatuna wauguzi wa kutosha kuweza kufanya kazi kote nchini,” alisema Tum.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa vyuo hivyo vimepiga hatua kubwa nchini tangu kuanzishwa kwake, ambapo serikali imefungua jumla ya vyuo 23 kote nchini tangu mwaka 2003 na kuongezeka idadi hiyo hadi 56.
Aidha, ametoa wito kwa wabunge na serikali za kaunti kuwekeza katika sekta ya matibabu ikiwemo ujenzi na upanuzi wa majengo katika vyuo vilivyoko kwenye kaunti.