Huku majira ya mvua yakiwadia nchini Kenya, wataalamu wa masuala ya afya na mashirika ya afya nchini Kenya wametoa onyo la kuwepo na mkurupuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
Haya ni kwasababu ya kufuatia ukosefu wa maji safi na kufeli katika kudumisha usafi wa mazingira.
Wataalamu hao wamesema kuwa iwapo mikakati dhabiti haitawekwa kuwaelimisha watu kuhusu umuhimu wa mazingira safi,usafi wa chakula na maji, basi idadi kubwa ya wakenya wako katika hatari ya kuathirika na maradhi ya kipindupindu.
Siku ya Jumanne, wizara ya afya ilitoa ripoti kuhusu hali ya mkurupuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambapo pia ripoti hiyo iliangazia kiundani kaunti 12 zilizoathirika na kwa wakati mmoja na ugonjwa wa kipindupindu.
Kaunti zilizotajwa ni pamoja na kaunti ya Nairobi, Nakuru, Siaya, Migori, Wajir, Marsabit, Tharaka Nithi, Tana River, Meru, Busia, Nandi na kaunti ya Garissa.
Kwa upande mwingine, shirika la madaktari wasio na mipaka MSF limesema kuwa hali ya usafi wa mazingira nchini Kenya wa sasa inaonyesha wazi kuwa kiwango cha maradhi ya kipindupindu nchini Kenya kitaongezeka. MSF imesema kuwa licha ya kuwa nchi ya Kenya imekuwa ikipigana vikali na athari za ugonjwa wa kipindupindu katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni dhahiri shahiri kuwa mikakati dhabiti iwekwe ili kudhibiti na kupigana na ugonjwa huo ambao ni hatari zaidi kwa wakenya.
Aidha, imebainika kuwa hata bila ya kuwepo na mvua baadhi ya maeneo kama vile mkoa wa Nyanza, bonde la ufa na kaskazini mashariki mwa nchi yanaathirika kwa pakubwa na ugonjwa huo wa kipindupindu.