Serikali ya Burundi imeahidi kushirikiana na Kenya katika uimarishaji wa biashara ya majani chai kama njia moja wapo ya kukuza uchumi wa nchi hizo mbili.
Makamu wa Rais wa taifa la Burundi Joseph Butore, alisema kuwa tayari mipango maalum ya kufanikisha biashara hiyo ya majani chai na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili imeidhinishwa.
Akiongea katika kongamano la wadau wa sekta ya majani chai nchini, lililoandaliwa mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Butore alisema kuwa kuna umuhimu wa wadau wa sekta hiyo kuweka bei ya jumla kwa bidhaa mbalimbali za majani chai wakati wa ukadiriaji wa bei, ili kurahisisha uuzaji wa majani chai katika mataifa ya magharibi.
"Kama taifa la Burundi, tuko tayari kushirikiana na Kenya kuimarisha biashara ya majani chai pamoja na uwekezaji baina ya mataifa haya mawili, ili kufanikisha biashara hiyo katika nchi za magharibi,” alisema Butore.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa Chama cha wafanyabiashara wa majani chai Afrika Mashariki Nicholas Mwinyi alisema kuwa watahakikisha kuwa biashara ya majani chai inaimarishwa kikamilifu.
Naibu rais wa Burundi atazuru magala mbalimbali ya majani chai nchini kubaini aina mbalimbali za majani chai na jinsi yanavyotengenezwa humu nchini.