Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya kitaifa inampango wa kuwekeza zaidi katika sekta ya uvuvi wa baharini, ili kupiga jeki zao la bahari katika uchumi wa taifa.

Akiongea kwenye kongamano la kamati ya bunge la kitaifa kuhusiana na ukulima, ufugaji na uvuvi mjini Mombasa, Waziri wa Ukulima nchini Willy Bett alisema serikali imetenga shillingi bilioni tatu kununua meli ndogo ya kasi.

“Meli hiyo itatumika kulinda sehemu ya maji makuu inayomilikiwa na taifa la Kenya ili kuilinda kutoka mikononi mwa wavuvi haramu,” alisema Bett.

Waziri huyo alisema kuwa kwa miaka mingi wavuvi kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika wamekuwa wakivua samaki katika maji makuu ya Pwani ya Kenya, na badaye kuwauza katika soko la humu nchini na mataifa mengine ya Afrika Mashariki.

Bett alisema kuwa hatua hiyo imefanya Kenya kupoteza mabilioni ya fedha kila mwaka.

Aidha, waziri huyo alisema kuwa serikali itanunua maboti ya kisasa yatakayo wawezesha wavuvi wa humu nchini kuvua samaki katika maji makuu ili kupanua soko la samaki nchini.