Huenda Kenya ikasitisha biashara ya uuzaji wa ngozi katika mataifa ya kigeni katika siku za hivi karibuni, kufuatia kushuka kwa mapato yanayotokana na biashara hiyo.
Akizungumza katika hoteli moja mjini Mombasa siku ya Jumatatu kwenye kongamano la ‘Regional Design Studio Project’, Waziri wa Viwanda na Ustawi wa Biashara Adan Mohammed alisema kuwa hatua hiyo imejiri kutokana na kupungua kwa ununuzi wa bidhaa zinazotengezwa na ngozi katika mataifa ya kigeni.
“Hakuna haja kushiriki biashara ambayo haina faida. Kama serikali tunalifikiria suala hilo na tunajadili na wadau husika kabla ya kuchukua hatua mahususi,” alisema Mohammed.
Aidha, waziri huyo alisema kuwa serikali inapanga kujenga kiwanda kikubwa cha ngozi katika eneo la Thika, Kaunti ya Kiambu ili kutengeza bidhaa mbalimbali za ngozi nchini pamoja na kubuni nafasi za ajira kwa vijana.
Kongamano hilo liliwaleta pamoja wanachama wa Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika COMESA.