Mke wa rais Margret Kenyatta amehimizwa kuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za akina mama haswa kwa maswala ya kijinsia katika nyadhifa za kazi ambazo hutolewa na serikali.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa akina mama hawakumbukwi katika nafasi za uteuzi kulingana na katiba.
Akizungumza siku ya Jumatatu mjini Nyamira, mwenyekiti wa chama cha Nyamira County Women Champions Edith Charanya amesema walianzisha chama hicho ili kutetea haki za akina mama na kuomba Kenyatta kujitokeza kuwasaidia katika kumiliki nafasi za uteuzi.
Kulingana naye wabunge hawajafanya yale yanayostahili kuwatetea wamama haswa katika masuala ya kijinsia ‘2/3 gender rule ‘ na kuomba usaidizi kutoka kwa Kenyatta ili wasonge mbele.
“Chama chetu ni cha kupeana mahitaji kwa serikali na tunaomba mama wa taifa kutusaidia ili wamama nao waweze kusikika katika taifa hili la Kenya,” alisema Charanya.
“Sisi wamama hatutaki kubaguliwa, kunyimwa haki za kupewa kazi, uongozi na mengine mengi ,” aliongeza Charanya.