Raisi Kenyatta katika mkutano wa awali. Kenyatta amekashifu hatua ya Nasa kutaka kususia marudio ya uchaguzi wa uraisi. Picha/buzzkenya.com

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Rais Uhuru Kenyatta amemshutumu kinara wa upinzani Raila Odinga kwa kuweka vikwazo vingi vinavyolenga kulemaza marudio ya uchaguzi wa uraisi.

Kenyatta ameitaja hatua ya vigogo wa Nasa kama isiyokuwa na manufaa kwa wakenya, bali kutaka kujinufaisha kibinafsi.

“Hawa jamaa wa vitendawili hawana  lengo la kuongoza taifa, bali wanalenga kuyanufaisha matumbo yao,”alisema Uhuru.

Akizungumza wakati wa mkutano uliowaleta pamoja takariban wajumbe elfu 15 wa chama cha Jubilee kutoka kaunti zote sita za pwani, Kenyatta alisema hatua ya Nasa kutaka kususia uchaguzi ni ishara ya kuogopa kushindwa.

“Wanajua tutawashinda, sasa wameanza kubabaika, tunawasubiri kwa debe Oktoba 26," alisema Uhuru.

Ameongeza kuwa njama ya Nasa ni kutaka  kuundwa kwa serikali ya mseto, ambayo serikali ya Jubilee haiko tayari kwa hilo.

Uhuru alisema kuwa chama cha Jubilee kiko tayari kwa uchaguzi na kwamba kama Raila hayuko tayari ana uhuru wa kujitoa  kwenye kinyanga’nyiro hicho.

Aidha, Kenyatta amewarai wajumbe hao kumfanyia kampeni mashinani ili kuibuka mshindi katika marudio ya uchaguzi.