Rais Uhuru Kenyatta Jumatano aliwasuta wawakilishi wa wadi katika kaunti (MCAs) kwa kuikashifu serikali kuu huku akisema viongozi hao wa wadi wamekuwa wakidai serikali kuu haijawekeza katika miradi ya maendeleo.
Kenyatta alisema serikali kuu hutoa mabilioni ya pesa kwa serikali za kaunti huku akisema ni ubinafsi kwa MCAs kudai wao ndio wamejenga zahanati na shule za chekechea katika maeneo ya mashinani ilhali fedha hizo hutolewa na serikali kuu kwa serikali zote 47 za majimbo.
"Baadhi yenu (MCAs) wamekuwa wakijigonga vifua kwamba wanafanya kazi, na serikali yangu haifanyi kitu. Mimi nawauliza, hizo pesa hutoka wapi? Hutolewa na serikali kuu," akasisitiza rais Kenyatta.
Akiwa pamoja na naibu wake William Ruto aidha walizidua ujenzi wa barabara ya Molo kuelekea Kibunja pamoja na ile ya Molo- Olenguruone.
Rais alisema kampuni moja ya Uchina itaweka lami barabara hizo na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa za ukulima katika maeneo bunge ya Molo, Kuresoi Kusini na Kuresoi Kaskazini.
Aidha rais Kenyatta aliwataka viongozi wa mrengo wa CORD kutumia mbinu starabu wanapoipinga serikali huku akiongeza kuwa serikali iko tayari kuongeza tume ya uchaguzi nchini fedha zaidi ili kuendelea kusajili wapiga kura."Tunaweka mikakati ya kuona jinsi IEBC itapata pesa zaidi, ili wakenya wengi wajiandikishe kama wapiga kura," Kenyatta alisema.
Rais alihutubia wakazi mjini Molo, Elburgon na Njoro huku akisema atazindua mashine za matibabu katika hospitali ya mkoa ya Nakuru mnamo Alhamisi mashine ambazo amesema zina thamani ya Ksh milioni 700.